Isaiah 6

Agizo Kwa Isaya

1 aKatika mwaka ule Mfalme Uzia alikufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu. 2 bJuu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao, na kwa mawili walikuwa wakiruka. 3 cNao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake: “Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu
ni Bwana Mwenye Nguvu Zote;
dunia yote imejaa utukufu wake.”

4 dKwa sauti zao, miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.

5 eNdipo nikalia, “Ole wangu! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana Mwenye Nguvu Zote.”

6 fNdipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni. 7 gAkanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa, nayo dhambi yako imesamehewa.”

8 hKisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”

Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”

9 i jAkasema, “Nenda ukawaambie watu hawa: “ ‘Mtaendelea daima kusikiliza,
lakini kamwe hamtaelewa;
mtaendelea daima kutazama,
lakini kamwe hamtatambua.’

10 kFanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu,
fanya masikio yao yasisikie,
na upofushe macho yao.
Wasije wakaona kwa macho yao,
na wakasikiliza kwa masikio yao,
wakaelewa kwa mioyo yao,
nao wakageuka, nikawaponywa.”

11 lNdipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?”

Naye akanijibu: “Hadi miji iwe imeachwa magofu
na bila wakazi,
hadi nyumba zitakapobaki bila watu,
na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,

12 mhadi Bwana atakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana,
na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.

13 nHata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi,
itaharibiwa tena.
Lakini kama vile mvinje na mwaloni
ibakizavyo visiki inapokatwa,
ndivyo mbegu takatifu
itakavyokuwa kisiki katika nchi.”
Copyright information for SwhKC